Kuwa mwekezaji makini?
Sisi kwenye Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana tunaamini kwamba uelewa wa mwekezaji unapaswa kutangulia uamuzi wa kuwekeza na kwamba ufahamu ni njia nzuri sana ya kumlinda mwekezaji. MWEKEZAJI MAKINI husoma taarifa muhimu za vitega uchumi alivyonavyo au anavyokusudia kuwekeza. Vilevile hutafuta ushauri wa uwekezaji toka kwa Washauri wa Uwekezaji, Wachuuzi, Madalali wa DSE na wataalamu wengine wenye leseni zinazohusika.
MWEKEZAJI MAKINI katika masoko ya mitaji anajua haki zake na anaelewa jinsi masoko ya mitaji yanavyofanya kazi. Ni muhimu kwa mwekezaji kujua mambo ya msingi na taratibu za bidhaa anazonunua kupitia masoko ya mitaji. MWEKEZAJI MAKINI hujifunza kuhusu masoko ya mitaji.
Mpango wa Kuwekeza
Kushinda vita ni lazima uwe na mpango wa vita. Ili kufanya ndoto zako za uwekezaji kuwa kweli, unahitaji mpango wa uwekezaji. Mipango ya uwekezaji humsaidia MWEKEZAJI MAKINI kupanga malengo yake ya kifedha na kufanyia kazi mpango huo ili kufikia malengo yake. Kuwa MWEKEZAJI MAKINI kwa kupanga shughuli zako za uwekezaji.
Hatari, Faida na Mwekezaji
MWEKEZAJI MAKINI huwa mwangalifu na hufikiria kuhusu hatari ya kupata hasara katika hatua yoyote ya faida. Kwa ujumla jinsi uwezekano wa kupata faida kubwa unavyoongezeka ndivyo jinsi hatari ya kupata hasara inavyokuwa kubwa pia. Kabla ya kutafuta vitega uchumi ambavyo vinaelekea kutoa faida kubwa fikiria hatari ya kupata hasara unayoweza kukumbana nayo pia.
MWEKEZAJI MAKINI haweki mayai yake yote kwenye kikapu kimoja. Njia mojawapo ya kupunguza hatari ya kupata hasara katika uwekezaji ni kuwa na mseto wa vitega uchumi kwa kuwekeza kwenye rasilimali tofauti.
Simamia Vitega Uchumii Vyako
Mpango wa uwekezaji unapopangwa na kutekelezwa haupaswi kuachwa bila kusimamiwa. Unatakiwa kuwa macho na mseto wako wa uwekezaji ili kujua maendeleo yake na ikiwa unahitaji marekebisho kulingana na hali halisi ya soko au maisha yako yanavyobadilika. MWEKEZAJI MAKINI siku zote anapanga lini aingie, atoke au abakie kwenye uwekezaji.